Sunday, August 26, 2012

Home Habari Matukio ya kusisimua Mtoto anusurika kifo mapigano Loliondo
Mtoto anusurika kifo mapigano Loliondo  Send to a friend
Sunday, 26 August 2012 09:00

Nkisheren Matangori akiwa Hospitalini baada ya kujeruhiwa.
Mussa Juma, Loliondo
MTOTO mmoja wa miaka 13, amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi begani katika mapigano ya jamii ya Wamasai wa ukoo wa Loita na Wasonjo(batemi) , yaliyoibuka hivi karibuni wilayani Ngorongoro.Nkisheren Matangori alijeruhiwa alipokuwa ndani ya nyumba yao kabla ya kundi kubwa la watu kuvamia kijiji chao na kuanza kuwashambulia kwa silaha na kuiba mifugo.
Akisimulia mkasa huo, mtoto huyo alisema  kuwa akiwa amelala  yeye, baba yake na  ndugu zake wengine, ilipofika majira ya saa 11 alfajiri walianza kusikia risasi zikipigwa ovyo kijijini.
“Mara kundi la watu wenye silaha lilifika katika nyumba yetu na kuanza kupiga risasi tulimokuwa tumelala na risasi moja ilinipiga juu ya mkono (begani), nyingine ilimpata baba,” alisema Matangori.
Alisema kuwa baada ya kupigwa risasi hiyo, alisikia moja ya nyumba yao, ikiwaka moto, huku kundi kubwa lingine likiendelea na uvamizi katika zizi la mifugo na kuanza kuchukua ng’ombe zaidi ya 500 na mbuzi zaidi ya 300 wa baba yake.
“Sikujuwa nini kimetokea kwani nilipata maumivu makali sana, ndugu yangu mwingine alipotoka nje kumbe alipigwa mshale na baada ya saa moja kijiji kilibaki kimya kuashiria wavamizi wameondoka,”alisema mtoto huyo.
Alisimulia kuwa baada ya kutolewa nje ya nyumba, ndipo alipata taarifa kuwa kundi kubwa la jamii ya Wasonjo(Batemi) ndiyo waliwavamia  ikiwa ni sehemu ya mgogoro wa ardhi ambapo wanawazuia wasiandikishwe katika Sensa katika kijiji cha Naan.
Mtoto huyo,  amelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Ngorongoro ya Wasso, akisubiri kuhamishiwa Hospitali ya Rufani ya KCMC mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi kutokana na hospitali hiyo kutokuwa na vifaa vya kuweza kuunga mkono wake, ambao mifupa kadhaa imesagika kutokana na risasi.
Wakati Matangori  kuhamishiwa KCMC, Baba yake Ketuko ole Matangori bado hajatolewa risasi katika mkono wake, ikielezwa kuwa anahitaji kufanyiwa upasuaji mkubwa ili kutoa risasi hiyo.
Daktari Festus  Kinabo wa Hospitali ya Wasso, anayewatibu Nkishereni na Ole Matangori, alisema kuwa hali ya mtoto huyo ni mbaya na mkono wake, hauwezi kutibiwa tena katika hospitali hiyo hivyo wanafanya utaratibu wa kumpeleka hospitali ya rufani ya KCMC.
“Picha za X- Ray zinaonesha mkono umesagika katika eneo la mifupa  mkubwa wa mkono na bado kuna risasi, hivyo tumeona ni busara kumhamishia hospitali ya KCMC,”anasema Dk Kinabo.
Kutokana na vurugu hizo, mifugo zaidi ya 1600 iliporwa na jamii ya Wasonjo na nyumba saba ziliteketezwa kwa moto, ambapo hadi jana vikao vya mwafaka kutaka kurejesha mifugo, vilikuwa vimekwama kutokana na jamii ya Kisonjo kuwa haijakubali kurejesha mifugo.
Tangu juzi viongozi wa Serikali na kisiasa wilayani Ngorongoro, wamekuwa na vikao na jamii ya Kisonjo, kutaka amani na kurejeshwa kwa mifugo, lakini bado mwafaka  haujapatikana hali ambayo inatishia kutokea mapigano zaidi.
Jamii ya Kimasai, tayari ilitangaza kutoa siku tatu, kurejeshwa mifugo hasa baada ya Serikali kuwataka wawe watulivu wakisubiri mwafaka na mifugo yao kurejeshwa.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!



7000 symbols left


Banner
Banner

No comments:

Post a Comment